 |
| Na Mwalimu Alfred Katuma. |
“5 Naam ,na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu,
Katika imani yenu tieni na wema na katia wema wenu maarifa……….”.
(1pet.1:5)
Bwana akufunulie akili zako ili uelewe hiki tunachojifunza lakini pia akusaidie kuyaweka kwenye matendo haya unayojifunza. Sasa hivi tunaishi kwenye nyakati ambazo kumezuka mafundisho yenye msisitizo mkubwa sana kwenye upande mmoja wa miujiza kiasi kwamba watu wengi sana wamejikuta wanaishi maisha ya kimiujiza miujiza,naamanisha watu wamekuwa wanaishi wakitegemea kufanikiwa katika maisha kwa miujiza tu unakuta mtu hataki kufanya kazi anategemea akienda kuwekewa mikono na watumishi basi mambo yatajileta yenyewe tu! Kwa sababu ya watu wengi kutaka kuishi kimiujiza wamejikuta kila kitu wanaita muujiza, unakuta mtu kafanikiwa kununua gari eti anaita muujiza au mtu kwenda ulaya anaita muujiza, mama kanunuliwa kanga na mumewe anaita muujiza.
Sijui kwa nini nimeanza kwa style hii lakini ninamini kuna kitu Mungu anataka tujifunze hapa na nianze kuelezea kuhusu muujiza. Ukisoma katika kamusi ya Kiswahili sanifu inafafanua neno muujiza kama jambo lisilokuwa la kawaida. Kwa maana nyingine muujiza ni matendo yanayofanyika kinyume na maumbile ya asili ni mambo ambayo hata ukimwambia mwanasayansi afafanue hawezi kuyafafanua yametokeaje, lakini utakuta mtumishi wa Mungu anamuombea mtu anasema ,”pokea muujiza wa kwenda ulaya! Pokea muujiza wa gari pokea muujiza wa nyumba! Na maombi mengine mengi ambayo ninaamini msomaji unayafahamu au umeshawahi kuombewa. Nisikilize nikwambie kama hayo maombi unayoombewa yangekuwa yanatokea, mfano unaambiwa pokea muujiza wa gari halafu gari inatokea from no where au ukienda nyumbani unaikuta gari imepark hujui ilikotoka haina mwenyewe basi huo ndo muujiza lakini ukichukua hela ukaenda mwenyewe kununua gari hapo kuna muujiza gani ndugu? Au unaombewa pokea muujiza wa kwenda ulaya halafu ghafla unajikuta uko ulaya hujui umefikaje huo nao ni muujiza.
Kitu gani nataka ujifunze hapa? Uache kuishi maisha ya kimiujiza kwa sababu mambo hayajileti yenyewe yanasababishwa kutokea,utanielewa tu huko mbele! Angalia Biblia yako nikuonyeshe mifano michache kuhusu miujiza halafu tuendelee, kutoka 7:10-12 inasema,
“10………Haruni akabwaga fimbo yake chini mbele ya farao,mbele ya watumishi wake,ikawa nyoka.
11Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi;na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo
Kwa uganga wao. 12Wakabwaga kila mtu fimbo yake,nazo zikawa nyoka;lakini fimbo ya Haruni
Ikazimeza fimbo zao”.
Sikia! hata ungewaita wanasayansi hapo hakuna ambaye angekueleza ile fimbo ya musa na za wachawi ziligeuka vipi zikawa nyoka! Huo ulikuwa muujiza lakini nataka ujifunze mambo machache hapa, kwanza fahamu Mungu anatenda miujiza lakini pia kama hufahamu shetani naye anatenda miujiza! Umeona hapo fimbo ya Musa ilipotupwa chini iligeuka nyoka na wachawi wa farao wakatupa zao nazo zikawa nyoka lakini (naupenda sana huu mstari) fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zile za wachawi! Unajua maana yake? Ni hivi, kile kitendo cha fimbo ya Haruni kumeza fimbo za wachawi Mungu alikuwa anamaanisha kwamba yeye ni mkubwa kuliko shetani,alikuwa anamaanisha muujiza wake ni mkubwa na unadumu kuliko wa shetani!
Ngoja niishie hapo Mungu akitoa nafasi nitakuja na somo linalohusiana na miujiza na Baraka maana hivi ni vitu vinavyowasumbua sana watu kiasi cha kuwafanya waishi maisha ya kutanga tanga kwa kuhama kanisa hili kwenda kanisa jingine. Sasa angalia maneno anayosema Mtume Petro wakati analiandikia kanisa waraka wake wa kwanza na ninachotaka uone hapo ni yale maneno anayosema “mkijitahidi kwa UPANDE WENU”! Sijui kama umeshawahi kutafakari mstari huu kwa makini na ukangundua yaliyojificha hapo; Petro anaposema kwa upande wenu ina maanisha kuna sehemu yako wewe kufanya kwa upande wako na kama kuna upande wako kufanya kitu basi pia kuna sehemu ya Mungu kufanya kwa upande wake na ndio maana kichwa cha somo kinasema mambo hayajileti yenyewe kwa sababu kuna kitu unatakiwa kufanya kwa upande wako ambapo ukikiunganisha na upande anaofanya Mungu unapata jibu lako! Ngoja twende na mifano, angalia yeremia 29:12 – 14 inasema hivi:-
12 Nanyi mtaniita,mtakwenda na kuniomba,nami nitawasikiliza.13 Nanyi mtanitafuta,na kuniona,mtakaponitafuta
Kwa moyo wenu wote.14 Nami nitaonekana,asema BWANA,nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa……………….”.
Kwa tafsiri rahisi ni kama Mungu anasema,kwa upande wenu mnachotakiwa kufanya ni kuniita,mnachotakiwa kufanya ni kuniomba na kwa upande wangu ninachotakiwa ni kuwasikiliza,na kujionyesha kwenu! Maana yake ni nini? Kama huiti Mungu hawezi kuitika! Ndiyo! Ataitikaje wakati hajaitwa? Mpendwa unakumbuka ule mstari ambao hata ukimuuliza mtu asiye na tabia ya kusoma biblia atakutajia mstari huo? Ni ule wa mathayo 7:7, hebu uangalie kwa namna hii nilivyofanya ili kukurahisishia kuelewa!
Upande wako kufanya kitu upande wa Mungu kufanya kitu
Ombeni nanyi (kuomba) mtapewa (kukupa unachoomba)
Tafuteni nanyi (kutafuta) mtaona (kukuonyesha unachotafuta)
Bisheni nanyi (kubisha/kupiga hodi) mtafunguliwa (kukufungulia malango)
Kumbuka mambo hayajileti yenyewe bali yanasababishwa kutokea na kwasababu hiyo hauwezi kufanikiwa katika jambo lolote kama utakuwa ni mtu wa kukaa na kusubiri Mungu afanye kitu na hata kama Mungu akifanya kitu amefanya kwa upande wake kama wewe hujafanya kwa upande wako hauwezi kupata matokeo! Angalia mfano huu nikuonyeshe kitu, fungua Yohana 9:6-7 inasema hivi,
“6 Alipokwisha kusema hayo,alitema mate chini,akafanya tope kwa yale mate.
Akampaka kipofu tope za macho,7 akamwambia,nenda kanawe katika birika ya Siloamu,
(maana yake aliyetumwa).Basi akaenda na kunawa;akarudi anaona”.
Hii ni habari ya mtu mmoja aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa na kwa bahati akakutana na Yesu lakini katika kuponywa kwake kuna kitu alitakiwa afanye kwa upande wake ili kukamilisha uponyaji wake na kilikuwa ni kwenda kunawa kwenye birika ya siloamu na biblia inasema akaenda na kunawa akarudi anaona! Kama yule kipofu angeamua kudharau akapitiliza na kuendelea na mambo yake mengine asiende kunawa ninakwambia angebaki kipofu hivyo hivyo lakini si kwa sababu Mungu hakufanya kitu,hapana, Mungu alishafanya kwa upande wake na ilibaki sehemu yake yule kipofu kufanaya ili kukamilisha uponyaji wake!
Okey! Angalia mfano wa mtu mmoja aliyekuwa na ukoma jina lake Naamani, huyu alimwendea mtumishi wa Mungu Elisha baada ya kusikia kuwa anaweza kumponya. Alipofika kwa Elisha,alitumiwa ujumbe wa mtu kumwambia kuwa aende katika mto Yordani akajichovye mara saba na ngozi ya mwili wake itarudi kuwa kawaida kabisa.
Naamani aliposikia hivyo alikasirika na kusema,”Tazama,nilidhania,bila shaka atatoka kwangu, na kusimama na kuomba kwa jina la BWANA,Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je abana na farpari,mito ya Dameski si bora kuliko mito yote ya Israel? Siwezi kujiosha ndani yake na kuwa safi? Akageuka akaondoka kwa hasira”.
(soma habari hii katika kitabu cha 2wafalme 5:9-14) Haya ndiyo mwazo waliyonayo watu wengi sana wanapokwenda kanisani au kwenye semina na mikutano ya neno la Mungu au wanapofanyiwa maombezi. Unakuta mtu haamini mpaka awekewe mikono na mtumishi, lakini nataka nikwambie kitu kimoja ambacho watu wengi wamekuwa wanakosea ambacho ni kutokuafuata maagizo wanayopewa na watumishi au kutofuata vile neno linavyosema. Sikia! Kama umeambiwa kanawe katika birika ya siloamu nenda kanawe! Kama umeambiwa kajioshe kwenye mto yordani, nenda kajioshe! Kama umeambiwa endelea mbele hata kama mbele yako kuna bahari, wewe endelea mbele!!! JUST DO IT! Upande wa Naamani ulikuwa ni kujiosha kwenye mto Yordani tu na hakuna kingine na ndio maana wale watumishi walimwambia maneno haya,”Baba yangu kama yule nabii angelikuambia kutenda jambo kubwa,usingalilitenda? Je si zaidi basi akikuambia,Jioshe uwe safi?” nachotaka kukuambia hapa ni wewe kufuata maagizo ya neno la Mungu linavyosema. Kwa hiyo nabii Elisha alifanya kwa upande wake na ulibakia upande wa muhitaji ambaye ni naamani, na lipokubalikufuata maagizo alipona kabisa!(haleluya!) Petro anasema mkijitahidi kwa upande wenu, (kumbuka hilo).